MPENDE ADUI YAKO

MPENDE ADUI YAKO
Mwanadamu ana asili ya Uungu ndani yake na hilo linamfanya awe na tabia ambazo hata Mungu anazo. Moja ya asili, tabia ama vitu vinavyomfanya Mungu awe Mungu, ni Upendo. Mungu ni Pendo na Pendo ni Mungu. Na kwa kuwa mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu uhakika ni kwamba ndani yake ana asili ya Upendo tangu wakati anaumbwa.

Nafahamu kwa dhati kabisa ni rahisi kusema nimemsamehe aliyenikosea kuliko kusema ninampenda. Lakini ukweli ni kwamba haya mambo mawili yanaenda pamoja na kimsingi kabisa upendo huanza kabla ya msamaha. Siyo jambo rahisi kumsamehe mtu usiyempenda, hilo halipo. Unasamehe kwa sababu unapenda. Unapenda ndiyo sababu unasamehe.

Na jambo hili lipo wazi kabisa kwa kuwa ndivyo Mungu mwenyewe alivyofanya. Alimpenda mwanadamu kwanza na ule upendo ukamsukuma kusamehe. Upendo una nguvu ya kuachilia msamaha. Ni ngumu sana na haiwezekani ukasamehe bila kuwa na upendo ndani yako. Hili halina njia mbadala. 

Kama kweli unataka kuwa mtu wa msamaha ni lazima ujue kuwapenda adui zako. Michakato yote na hatua zote zitawezekana iwapo tu umejua kupenda na hatimae msamaha utaachiliwa.

Anza leo kampeni maalum ya kuwapenda adui zako. Unasamehe kutoka kwenye upendo. Inawezekana adui yako ni wewe mwenyewe ama tabia fulani ambayo huipendi na inakuumiza. Unataka kusonga mbele, suluhu ni kujipenda na baadae unajisamehe. 

Inawezekana adui yako ni mtu mwingine aliyekuumiza na umembeba kila siku katika moyo wako, umebeba uchungu na maumivu, kama unataka umsamehe na kutoendelea kumbeba ndani ya moyo wako anza kumpenda leo na hatimae utajikuta siku moja umeachilia msamaha juu yake. 
Anza kampeni maalum ya kuwapenda adui zako.

Kumbuka: "Msamaha sio kutetea wala kuhalalisha kwamba kilichofanyika kilikuwa sahihi."

Tukutane Alhamis ijayo...

#SAMEHE, ISHI SALAMA






Goodluck Ernest, 2016
+255 713 660921
 mashambo.ge@gmail.com
Previous
Next Post »