UNAWEZAJE KUTENGENEZA NA KUKUA KATIKA MSAMAHA
(Sehemu ya Nne)
Ni chaguo la mtu binafsi kuamua kujifunza, kutengeneza na kukuza tabia ya msamaha. Ni jambo linalohitaji maamuzi ya mtu mwenyewe. Na ni ukweli pia kwamba huu ni mchakato unaohitaji muda ili kufanya tabia ya msamaha na moyo wenye kusamehe kuwa sehemu ya maisha yako. Swali ni Je, utaufanyaje mchakato huo uendelee?
Jambo la Nane:
Weka Mkakati wako wa kujiboresha katika Msamaha na Kusamehe.
Wanadamu tulivyoumbwa, tumeumbwa katika namna ambayo kila kitu katika maisha yetu kinaweza kukua. Kila jambo kwenye maisha yetu kinaweza kutembea na kusogea.
Sasa, hata kama kisiposogea maana yake kwa dhati kabisa siyo kwamba hakijasogea bali kimerudi nyuma. Hakuna kubaki mahali pamoja (kwenye asili ya uumbaji wetu). Ni mambo mawili tu hapa, ama unakua kwa kwenda mbele ama unakua kwa kwenda nyuma (hukui).
Hivyo kama ambavyo unaweza kuifanya tabia yako ama hali yako nyingine kuwa bora zaidi basi fahamu hata tabia ya kusamehe na moyo wa msamaha huweza kukuzwa na kuwa bora zaidi. Weka mkakati wako binafsi wa kuiboresha tabia hii.
Ichochee ili iende mbali zaidi ndani ya moyo wako. Ifanye iwe dhahiri kila siku katika maisha yako.
Ikuze na ifikie watu waone msamaha badala ya kukuona wewe. Ifanye kuwa bora zaidi.
Weka mkakati na utembee katika mkakati huo. Kwa kuwa utakapoacha kuikuza si ajabu ukajikuta siku moja kumbe ulishaacha kabisa kusamehe ingawa kabla ulikuwa na tabia hiyo. Huu ni mchakato wa maisha, wa kila siku. Boresha.. Boresha.. Boresha.. Hakuna mwingine awezaye kufanya hivyo isipokuwa wewe mwenyewe. Weka mkakati huo sasa.
Jambo la Tisa:
Jizoeze kusamehe kila siku.
Kati ya mambo ambayo yatakusaidia kutengeneza tabia ya kusamehe ni kufanya mazoezi ya kusamehe kila siku hata katika yale mambo ambayo ungedhani si muhimu. Ni zoezi dogo sana lakini lenye linaloweza kutengeneza msingi bora na imara kwenye maisha yako.
Kwa mfano, inawezekana umechelewa kuamka na kwa bahati mbaya ukaona umechelewa kazini ama mahali ulipopanga kwenda. Sasa unajikuta unajiandaa kwa haraka huku una maumivu na kujilaumu ndani yako. Lakini ukiamua kuichukulia hiyo kama fursa ya kujifunza msamaha basi unaanza kuachilia msamaha, unajisamehe na kuamua kuwa na furaha ndani yako. Ni rahisi hivyo.
Vile vitu vidogo vidogo tena vya kila siku vinakupa nafasi ya kufanyia mazoezi tabia yako ya msamaha. Labda upo unatazama televisheni na ni kipindi kizuri sana unachokipenda na ghafla umeme unakatika. Mara nyingi utajikuta unapata hasira hata kama ni ndogo ama unapata uchungu fulani hivi.
Hiyo ni fursa ya kuchochea, kuitengeneza na kukuza tabia ya msamaha ndani yako. Unaamua kusamehe na kuachilia haraka. Badala ya kunung'unika ama kuumia ndani yako unaamua kuwasamehe ama kujisamehe labda kwa sababu ulisahau kununua luku. Unaachia msamaha.
Vipo vitu vingi vidogo vidogo tena vinavyotuzunguka kila siku, vinavyoweza kutumika kama fursa ya kuichonga na kuitengeneza tabia ya msamaha ndani yako. Zitumie na usichoke kuweka kwenye matendo.
Kumbuka: Msamaha ni kukubali kwamba hakuna ambacho utakifanya kumuadhibu aliyekuumiza ili uweze kupona majeraha aliyokusababishia yako.
Tukutane Alhamisi ijayo..
#SAMEHE, ISHI SALAMA
Goodluck Ernest,
September 7th, 2016
+255 713 660 921
mashambo.ge@gmail.com
Sign up here with your email
1 comments:
Write commentsMungu akutie nguvu
ReplyConversionConversion EmoticonEmoticon