MSAMAHA WA KWELI KATIKA UPENDO

Na Goodluck Ernest
Kilichomfanya Yesu asiondoke msalabani si misumari aliyokuwa amepigiliwa. Msalaba wala misumari havikuwa na uwezo wa kumshikilia Yesu kwa namna yoyote ile. Ni Yesu huyo huyo aliyeuumba mti uliomtundika. Alikuwa na uwezo wote wa kutoka pale. Lakini UPENDO ulimshikiza Yesu msalabani. Upendo ulimzuia Yesu msalabani. Upendo ulimnyamazisha Yesu msalabani. Upendo ulimpa uvumilivu na utii Yesu. Upendo ulimyenyekeza Yesu mpaka alipofanikisha mpango na mradi mzima wa Msamaha kwa mwanadamu.
Kumbe kuna nguvu katika Upendo. Na moja ya nguvu ambayo imefungwa katika Upendo ni Msamaha. Si tu kwamba ni vigumu lakini pia haiwezekani kusamehe ikiwa hakuna upendo ndani yako. Upendo ulimsukuma Mungu kukubali kuingia gharama na kumsamehe mwanadamu hata kabla mwanadamu huyo hajaomba msaada wa kusamehewa. Ilimgharimu maisha yake, ilimgharimu mateso, ilimgharimu kuacha utukufu wake, ilimgharimu kudharauliwa na kutoheshimiwa ili tu aweze kufikia hatua ya Msamaha kwa mwanadamu. Upendo!
Usitumie nguvu kubwa sana kusamehe. Tafuta kwanza kupenda. Funguo za msamaha zimefichwa katika upendo. Pale ambapo utaweza kupenda ndipo utashangaa ilivyo rahisi kusamehe. Tutakapotaka kuona una upendo kiasi gani ndani yako tutatazama unaweza kusamehe kwa kiasi gani. Unapotaka kujua una upendo kiasi gani ni rahisi tu, tafuta kuona unaweza kusamehe kiasi gani.
Kumbuka: _Upendo hutangulia Msamaha_
Tukutane Alhamisi ijayo...


#SAMEHE, ISHI SALAMA
Goodluck Ernest, The Diplomat
mashambo.ge@gmail.com
+255 713 660921

Previous
Next Post »