UNAWEZAJE KUTENGENEZA NA KUKUA KATIKA MSAMAHA 
(Sehemu ya Kwanza) 

Kila siku unahitaji kujifunza na kukuza moyo wenye kusamehe. Kuwa na moyo wenye kusamehe ni mchakato na haitatokea kwa ghafla tu. Ni lazima ujitahidi kila siku kuutengeneza na kufanyia kazi ili hatimaye kuwa na moyo unaoachia msamaha bila kujali mazingira na tabia ambazo labda zinaweza kuwa kikwazo cha wewe kutoa Msamaha. 

Yapo mambo ambayo unaweza kuyafanya ili kuitengeneza tabia hii. Haya hapa ni baadhi tu kati ya mengi na si yote. 

Jambo la Kwanza: Mweleze Mungu, umtegemee na umwamini yeye kukufundisha kusamehe. 
Ni kweli kibinadamu si rahisi kabisa kuweza kusamehe. Siyo jambo rahisi kuwa na tabia ya kusamehe. Lakini yupo Mungu ambaye ndiye mwanzilishi wa msamaha na ni yeye awezaye kukufundisha kusamehe, mtafute huyo. Mtegemee yeye na umwamini kwamba hatimaye anaweza kukusaidia ukawa na tabia ya kusamehe. Kuwa na muda wa kuombea hilo kama ambavyo huwa unaombea kazi, ndoa, biashara na hata familia yako, basi sasa ombea na tabia. Usichoke kuomba hata pale unapoona mbona bado nashindwa, endelea kuomba. Jifunze neno la Mungu linasemaje juu ya Msamaha na hatimae taratibu litakubadili na kuanza kuwa na moyo wenye kusamehe. Usichoke wala kukata tamaa. 

Jambo la Pili: Tafakari ujue ni kwa nini unahitaji kusamehe zaidi. 
Katika hali ya kawaida lazima uwe na sababu ya kufanya jambo. Haiwezekani ukataka kuwa na moyo wa kusamehe wakati hujui ni kwa nini yakupasa kusamehe. Kaa chini na tafakari faida za kusamehe na hasara za kutosamehe. Tafakari ni kwa nini Mungu ametoa amri ya kusamehe na kwa nini anataka tusamehe. Tafakari kila siku. Chukua muda wako uone kwamba msamaha ni nini. Katika tafakari yako angalia na fuatilia uone kile ambacho neno la Mungu linasema kuhusu Msamaha. Iwe ni muda wa kujua ni kwa nini unahitaji kusamehe, kwa nini unatakiwa kuendelea kusamehe zaidi na zaidi. 

Kumbuka: Upo uwezekano wa kukosewa kila siku. Hivyo ili usibebe maumivu na chuki kila siku basi Msamaha nao ni maisha." 

Tukutane Alhamisi ijayo..
#SAMEHE, ISHI SALAMA





Goodluck Ernest,
August 18, 2016
+255 713 660921
mashambo.ge@gmail.com
Previous
Next Post »