Mara nyingi Msamaha unapozungumziwa imekuwa unazungumziwa kutoka kwenye jicho la aliyekosewa. Na yapo mambo mengi ambayo yamesemwa ili ufanye ikiwa umekosewa na kuumizwa. Lakini, Je kama wewe ndiye uliyekosa na unahitaji msamaha unafanya nini?
Hatua ya kwanza ni Kujifanyia tathmini na kukubali kwamba umekosea na makosa uliyoyafanya yamemuathiri mwingine. Hili ni muhimu sana. Lazima ufahamu kwamba umekosea na umejeruhi mtu mwingine. Tafuta na uone ni wapi ulipokosea, uone ni wapi ambapo hukufanya sawasawa na matokeo yake ukasababisha majeraha kwa mwingine.
Baada ya kujichunguza na kujua kwamba ni kweli umekosea sasa iendee hatua ya pili ambayo ni ukiri wa kosa ulilofanya kwa yule uliyemkosea. Ni muhimu sana ufanye ukiri tena ulio wa dhati kwamba umekosea na kujeruhi. Kama unataka msamaha wa kweli ni lazima ukiri na kuomba msamaha. Zungumza kwa mkosewa kuhusu huzuni yako na kujutia kwako kwa ajili ya kosa lililofanyika.
Baada ya ukiri wa kosa basi hatua inayofuata ni kuomba msamaha. Omba msamaha bila kutengeneza sababu sababu(excuses), usizitafute. Wewe baki kwenye nia yako ambayo ni kuomba msamaha. Kuwa mkweli na usitafute kujitetea kwa namna yoyote katika kuomba kwako msamaha.
Unapomaliza kuomba msamaha ni muhimu basi wewe mwenyewe upite kwenye hatua ya kujisamehe pia. Usibaki kwenye kujihukumu na wala kubaki na hatia. Ni lazima na ni muhimu sana kuachia msamaha kwako wewe mwenyewe ili uwe tayari pia kupokea msamaha kutoka kwa mkosewaji.
Mwisho na muhimu sana, ni kukubali na daima ukumbuke kwamba huwezi kumlazimisha mtu akusamehe. Hata baada ya kuomba msamaha siyo lazima yule uliyemuomba msamaha akusamehe hapo hapo. Siyo sahihi kumlazimisha uliyemkosea akusamehe. Uamuzi wa kusamehe ni wake na siyo wako. Wengine huhitaji kuuelekea msamaha kwa muda wao. Siyo lazima asamehe katika muda unaotaka wewe.
Matokeo yoyote yale baada ya kuomba msamaha, wewe songa mbele na mwachie Roho Mtakatifu ashughulike na mkosewa na zaidi wewe endelea kumwombea..
Tukutane Alhamisi ijayo...
#SAMEHE, ISHI SALAMA
Goodluck Ernest
+255713660921
mashambo.ge@gmail.com
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon