UNAWEZAJE KUTENGENEZA NA KUKUA KATIKA MSAMAHA (Sehemu ya Tatu)

Mfumo wa maisha tunaouishi kila siku, unatufanya tusiwe na chaguo jingine zaidi ya kujifunza msamaha na kusamehe na hatimae kila siku kuifanya kuwa tabia na sehemu ya maisha yetu. Swali la msingi sana hapa ni Je, unawezaje kuitengeneza tabia hii na kuifanya ikue ndani yako?

Jambo la Sita:
Punguza tabia hasi, Stawisha wema ndani yako.
Tabia, fikra, mawazo na sifa hasi zipo na zitaendelea kuwepo na ni jambo muhimu sana kushughulika nazo kama unataka kutengeneza moyo wa msamaha na tabia ya kusamehe ndani yako. Shughulika na kuzipunguza tabia/sifa/fikra hasi kila siku (kwa kuwa huu ni mchakato) ndani yako. Usikubali ziendelee kukua na kukomaa ndani yako.

Kwa kufanya hivyo ni rahisi sasa kuacha nafasi kwa tabia, sifa na fikra sahihi kuweza kuingia ndani yako. Amua sasa kukuza na kustawisha mema na fadhila ndani yako. Na haiwezekani kufanya hivyo wakati moyo, akili na nafsi yako vimejaa mambo hasi tu. Amua kwa dhati kuziondoka taratibu lakini kila siku. Na chochea mema, wema na uzuri ulionao ama ambao ungetamani kuwa nao.

Ni jambo linalowezekana kabisa. Ukiweza kutoa tabia hasi ndani yako ni rahisi sasa kuweza kuachilia msamaha. Mtu anapokukosea ama kukuumiza bado unaweza kuona nafasi ya kumsamehe kwa kuwa tayari ndani yako kuna mbegu ya fadhila na wema. Lakini ikiwa tayari una ubaya ndani yako kitakachokutoka ni uchungu na kisasi kwa sababu hiyo ndiyo mbegu iliyopo ndani yako.

Jambo la Saba:
Badilisha uzoefu wako wa zamani.
Mara nyingi tumeendelea kuishi katika uzoefu wa yale tuliyopitia nyuma. Ni muhimu sana kujua kwamba siyo uzoefu wote ambao tumepitia nyuma unafaa kuendelea nao hata tunapoiishi leo yetu. Inapofika kwenye Msamaha na Kusamehe ni lazima ukubali kubadili uzoefu wako wa nyuma na ukubali uzoefu mwingine. Unaishi leo na siyo juzi. Uliumizwa jana, ni sawa lakini hakuna faida yoyote ya wewe kuishi uzoefu wa maumivu ya jana leo. Una majeraha ni kweli, lakini hupaswi kuishi uchungu wa jana leo. Badili uzoefu.

Kuna jambo jipya na jema zaidi ya jana. Leo kuna uzoefu mpya na mwema kwako unaopaswa kuuishi. Na uzoefu huo upo kwenye kusamehe. Amua kuacha ile habari ya jana, kuna habari njema kwako hivi leo. Kama unataka kuipata, kuipokea kuiishi habari njema hiyo basi badili uzoefu wako wa jana na samehe kisha anza kufurahia uzoefu huu mpya.

Ni lazima ukubali na uamue kila siku kuondoa uzoefu wako wa maumivu na majeraha ya zamani na kukubali kuishi leo ili uweze kukua katika msamaha na kusamehe. Vinginevyo usipofanya hivyo ni rahisi kuona majeraha a maumivu uliyopitia na hatimae kubeba uchungu na kisasi tu. Na kufikia hapo huwezi kujenga tabia ya kusamehe wala moyo wa msamaha ndani yako.

Tukutane Alhamisi ijayo...

#SAMEHE, ISHI SALAMA
Goodluck Ernest, 2016
+255 713 660921
mashambo.ge@gmail.com
Previous
Next Post »