MSAMAHA WA KWELI - 2

Halisi ya Msamaha wa kweli ni ule wenye gharama. Haiwezekani msamaha ukawa halisi halafu ikawa rahisi tu kuutoa. Lazima atoaye agharamike. Utaona ameumizwa na kweli ana haki katika lililotokea. Lakini kwa kuwa Msamaha ni gharama inamlazimu kukubali kuuachia haki yake ili mkosaji aupate msamaha. Na hilo la gharama linaenda pamoja na Mpokea Msamaha kupokea bila kulipa chochote. Anapokea bure tu pamoja na gharama zote alizoingia Mtoa msamaha. Huo ndiyo Msamaha wa kweli. 
Lakini chini ya hayo mawili kuna mengine ambayo ni: 3. Hauchagui:
Msamaha wa kweli hauna uchaguzi wa nani wa kusamehewa na nani hapaswi kusamehewa. Msamaha wa kweli hauna upendeleo kwa watu fulani na fulani. Kimsingi msamaha ni kwa ajili ya aliyekosea. Hivyo ili msamaha uwe halisi na wa kweli ni lazima uondoe uchaguzi wa nani wa kumsamehe. 

Ndiyo sababu ingekuwa maajabu mbinguni na duniani kama Yesu angechagua kuwasamehe wakristo tu. Nina uhakika hata Mungu mwenyewe asingekubali kuingia hiyo gharama ya kumleta msalabani. 

4. Mkosaji hakustahili kuupata:
Msamaha wa kweli na halisi kwa hakika kabisa huwa haumstahili yule anayepewa. Hapa ni muhimu sana. Kimsingi, Msamaha wa kweli ni ule ambaye yule aliyekosea hastahili kabisa kuupokea lakini anapewa hivyo hivyo. Ndiyo. 

Ukitaka kujua kama huu msamaha ni wa kweli ama la, utaona katika kutafuta kila sababu ya kusamehe na sababu hiyo haipatikani. Utaona mazingira yote yanaonyesha jambo sahihi kufanya hapo ni Adhabu, Kisasi, Hukumu. Hutaona kingine. Hata hivyo nyakati kama hizo ndiyo Msamaha wa kweli huonekana. Msamaha wa kweli humtafuta yule asiyestahili. 

Najaribu kuwaza Msamaha ungekuwa unatafuta anayestahili, labda Yesu angeweza kufika msalabani halafu ghafla akaghairi zoezi zima. Lakini aliendelea na kuikamilisha kazi ya msalaba kwa kuwa alijua kwa hakika ya kwamba Msamaha wa kweli huenda kwa yule asiyestahili. 

Tukutane Alhamisi ijayo...

#SAMEHE, ISHI SALAMA
Goodluck Ernest, 2016
+255 713 660921
mashambo.ge@gmail.com
Previous
Next Post »