Ukweli wa kilichotokea msalabani (Sehemu ya 2)

Na Daniel L. Mganga.


Kitu kingine ambacho kilitokea msalabani na kanisa halijakielewa vizuri ni upya wetu mpya.

Ukweli ni kwamba wokovu hauishii kwa wewe kuoshwa dhambi zako zote msalabani, kuna kitu cha muhimu tunakisahau..
*Tulikuwa tumekufa,* hatuna uhai wowote, wala tumaini kama walivyo ambao hawajazaliwa upya.

Waefeso 2:4-6

*Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu Aliyotupenda, hata kwa wakati ule tulipokuwa WAFU kwasababu ya makosa yetu* *Alituhuisha pamoja na Kristo, yaani tumeokolewa kwa Neema.*
*Akatufufua pamoja naye, Akatuketisha pamoja naye katika ulumwengu wa roho, katika Kristo Yesu.*

Mungu kupitia msalaba ametuzaa upya, tumekuwa viumbe vipya vilivyo na uhai wake.

2 Wakorintho 5:17

*Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama yamekuwa mapya*

Si kwamba Yesu alitufufua na kutupa uhai wa Mungu (uzima wa Mungu), bali ametufanya kuwa viumbe vipya ndani yake. Ukweli ni kwamba hauna historia na kwa hiyo laana ya Adamu haikuhusu, baraka za mwenye Haki ndani ya Kristo ni Haki yako.

Ni muhimu kujua kwamba kuwa ndani ya Kristo, si kukiri tu na kufutiwa makosa, ila ni kuzaliwa katika upya wa utukufu mkubwa, tulikufa na kuteswa pamoja na Kristo msalabani na utukufu lionao sasa ametupa.

Ule utu wetu wa zamani, uliokuwa unahusiana na Mungu kisheria umekufa pale msalabani. Sasa hivi tunayo asili ya Mungu ndani yetu.

Waefeso 2:10

*Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo*

Mungu ametutengeneza upya katika Kristo na ametuandalia asili ambayo katika hiyo tutatenda yaliyo mema, ametufanya kuwa Haki yake ( 2 Wakorintho 5:21).

Hivyo ni vyema kujua kuwa wewe si yule wa zamani, ulikuwa umekufa kupitia mauti ya Yesu Kristo. Ulikufa na kufufuka pamoja nae. Lakini haikuishia hapo. Amekupa asili ya haki yake. Wewe ni kiumbe kipya, kisichokuwa na mawaa. Unaweza usijione hivyo katika mwili lakini ndivyo ukweli ulivyo, rohoni mwako umefanyika kuwa kiumbe kipya. Ya kale yamepita kabisa!

Usipofahamu haya, mwili  utakusumbua kwa kuonesha uhalisia wa asili ya dhambi ilhali asili hiyo ilishakufa. Wakorintho walipokosea katika mwenendo, mtume Paulo aliwauliza "Je hamjui miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu?!"
Kutojua kwao ama kutozingatia ukweli wa kile kilichofanyika, vilihusiana sana na makosa yao.

Ni muhimu sana kujua uhalisia wa upya wako ndani ya Kristo, si kwamba umebadilishwa, hapana umezaliwa upya kwenye familia ya Mungu, wewe ni mtu wa milki ya Mungu, mwenyeji wa mbinguni.
Dhambi imewekwa chini ya miguu yako.

Kiumbe kipya ndani ya Kristo!


Previous
Next Post »