USIKATE TAMAA



Kabby ni kijana wa kitanzania ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Nyabisindu. Ni moja kati ya vijana waliobahatika kusoma kati ya watoto kumi na mbili wa mzee Bikolahasi. Alianza safari yake ya Elimu ya msingi katika shule ya msingi Nyabisindu. Akiwa darasa la nne tu, familia yake iliyokuwa inaonekana kujiweza kijijini pale ilipata pigo kubwa baada ya wazazi wake kugongwa na roli wakiwa wamebebana kwenye baiskeli wakitokea sokoni Mkadunduli walikokuwa wametoka kufanya biashara. Wakiwa wanakimbizwa hospitali ya wilaya, walipoteza maisha wote wawili.
Lilikuwa ni pigo kubwa kwa kijana Kabby. Akiwa kaka mkubwa alikuwa na wajibu sasa wa kuwatunza wadogo zake. Kabby alipata wakati mgumu sana. Aliwaza sana cha kufanya lakini hakuwa na majibu. Akiwa amekaa peke yake anatafakari alikumbuka maneno ya baba yake enzi za uhai wake... ```"Siku zote usikate tamaa, pigana kiume hadi uone tone la mwisho, yaani tone la damu. Pia kumbuka matatizo yanapokuja yanaifanya akili yako ijifunze mambo mengi. Kuwa na akili mwanangu siyo kukaa na kulalamika tu."```
Ghafla alipata nguvu ya kusonga mbele, aliamua kutafuta namna ya kuishi. Pale nyumbani kwao walikuwa wanajishughulisha na biashara ya kuuza pombe ya kienyeji aina ya Rubisi. Kijana Kabby aliendeleza ile biashara na kidogo mahudhurio yake shuleni yalianza kufifia. Wadogo zake waliokuwa kama mapacha vile kwasababu ya kutofuata uzazi wa mpango, tayari walikuwa shule. Watatu walikuwa darasa la tatu, wawili darasa la pili, wawili darasa la kwanza huku wengine wanne walikuwa bado hawajaanza shule. Kabby alifanikiwa kufaulu mtihani wa darasa la nne na kuingia darasa la tano. Lakini mahudhurio yake yalikuwa mabaya mno, kwani alikuwa akihangaika huku na kule ili wadogo zake wapate chochote cha kuwasogeza.
Baadae aliamua kuacha shule kabisa baada ya mdogo wake wa mwisho kufariki baada ya kupatwa na utapiamlo. Aliendelea kusota mtaani huku akifanya kila shughuli halali ambayo ingeweza kumwingizia kipato. Aliwasaidia wadogo zake wakapata chakula na mahitaji mengine muhimu.
Alifanikiwa kuwasomesha wadogo zake hadi wale wawili waliokuwa nyuma yake walipo hitimu masomo yao ya shule ya msingi. Matokeo yalipotoka mmoja alifaulu kwenda kidato cha kwanza shule ya sekondari Kisonori mkoani. Yule ambaye hakufaulu aliendeleza biashara zilizoanzishwa na Kabby, na huku Kabby akaamua kurudi darasani. Aliendelea na darasa la tano, huku wadogo zake wakiwa wametangulia mbele yake. Alifurahi kuona hivyo, pia alifurahi kurudi shuleni.
Alisoma kwa juhudi sana na kwa nguvu kubwa sana. Mitihani yote alikuwa anafaulu sana, kulingana na uwezo wake, walimu waliamua kumharusha darasa na kuweka darasa la saba alipokuwa darasa moja na wadogo zake wawili.
Mtihani wa darasa la saba yeye tu kwenye hilo darasa ndiye aliyeweza kufaulu na kujiunga na kidato cha kwanza. Wakati huu mdogo wake alikuwa anaingia kidato cha nne. Wale wadogo zake waliofeli waligoma kurudi shuleni, baadae wale wawili waliomaliza na kaka yao waliamua kwenda zao mjini kutafuta kazi. Huku yule mwingine akiendelea na biashara pale kijijini na kuwasaidia kaka zake hela za matumizi na ada.


Previous
Next Post »