UNAWEZAJE KUTENGENEZA NA KUKUA KATIKA MSAMAHA (Sehemu ya Pili)


Hakuna mwanadamu aliye kamili na asiyekosea. Na kwa sababu hiyo kukosea na kukosewa ni jambo ambalo laweza kutokea kila siku katika safari ya maisha. Ni jambo ambalo hutaweza kulikwepa mara zote. Hivyo ni muhimu sana kujifunza na kukua katika msamaha. Ni vyema kupita katika mchakato huu kila siku ili kuitengeneza tabia hii ya Msamaha. Sasa ni mambo gani utakayoweza kuyafanya ili kuitengeneza tabia hii:

Jambo la Tatu:
Samehe Jeraha moja kwa wakati mmoja.
Wakati mwingine yaweza kutokea ukawa umeumizwa na mambo kadha wa kadha, zaidi ya jambo moja. Sasa jifunze kushughulika na jeraha moja kwanza kabla ya kuliendea jingine. Jenga tabia ya kushughulika na jambo moja baada ya jingine. Inawezekana umeumizwa kwenye mahusiano, ukalibeba hilo. Kabla jeraha hilo halijapona ukakuta umeumizwa kazini, na kadhalika na kadhalika. Inapotokea hivyo ni vyema basi usijaribu kusamehe kwa ujumla wake. Shughulika na kusamehe moja moja. Ni rahisi kutembea hatua moja kuelekea 2 na 3 kuliko kutaka kutembea hatua 5 kwa mara pamoja.

Jambo la Nne:
Watambue mashujaa wa Msamaha.
Kuna watu ambao wamewahi kuumizwa na kuachwa na majeraha makubwa tena yawezekana kuliko hata yale ambayo yatakupata wewe lakini hatimaye waligundua nguvu ya msamaha na kusamehe. Ni vyema ukafanya jitihada za makusudi za kuwajua na kuwatambua na kujifunza kutoka kwao. Kupitia uzoefu na habari zao kuna mengi ambayo kila siku utajifunza na kuweza kutiwa moyo. Ni wakati ambapo utaweza kupata taarifa, maarifa na ufahamu wao juu ya Msamaha na Kusamehe na kutokea hapo ukajitengenezea tabia ya kusamehe na moyo wa msamaha. Watafute na uwatambue mashujaa hawa. Wapo mashujaa wa msamaha wa mambo mbalimbali. Tumia muda wako vizuri kuwatambua na kujifunza kwao.

Jambo la Tano:
Jichunguze.
Hapa ni mahali muhimu sana kama kweli unataka kutengeneza tabia ya kusamehe. Ni hatua muhimu mno kama unataka kuutengeneza moyo wenye kuachilia msamaha. Jichunguze na kuwa mkweli kwako wewe mwenyewe na uujue udhaifu wako ni upi na nguvu zako ni zipi.  Jifanyie tathmini wewe mwenyewe. Tambua ni wakati gani unaweza hata wewe mwenyewe kumuumiza mwingine pengine labda kutokana na madhaifu uliyonayo. Jichunguze uone ni mara ngapi kwa kujua ama kutojua uliumiza ama umeumiza wengine. Jichunguze uone ni mara ngapi umekuwa unaumia mara baada ya kugundua ulikosea wengine. Kuwa mkweli na nafsi yako. Kama mwanadamu ni lazima utakuta kuna mahali ambapo umekuwa ukikosea, umekuwa ukijeruhi wengine. Nasisitiza tena jichunguze. Na huo ni mchakato wa kila siku. Endelea kufanya hivyo. Na hatimaye utagundua kumbe hata wewe mwenyewe unahitaji kusamehewa. Na kama kweli wataka kusamehewa ni budi nawe ujue kuwasamehe wengine.

Kumbuka: Samehe ili usamehewe

Tukutane Alhamisi ijayo...

#SAMEHE, ISHI SALAMA
Goodluck Ernest, 2016
+255 713 660 921
mashambo.ge@gmail.com
Previous
Next Post »