Msamaha

Na Goodluck Ernest 
Image result for forgiveness
Swali:
INAKUWAJE PALE AMBAPO MIMI AMBAYE NILIMKOSEA MTU SINA MAWASILIANO NA HUYO MTU, PENGINE HATA ALIPO SIPAFAHAMU AU HATA AMEFARIKI LAKINI NINA SHAUKU YA KUMWOMBA MSAMAHA, NIFANYE NINI? SI UNAJUA HATA MIE NIKIWA SINA UHAKIKA KAMA NIMESHASAMEHEWA INATESA..??

Majibu:
Kumtafuta mtu kuongea nae kuhusu kumsamehe ama kusameheana hiyo ni hatua tofauti kabisa na Msamaha. Hiyo ni hatua iitwayo USULUHISHI (RECONCILIATION).

Ni hatua inayokuja baada ya Msamaha lakini isiyo ya lazima. Msamaha waweza kuwa halali na wa kweli bila hata kufikia hatua hiyo. Hivyo suala ni KUMSAMEHE ikiwa Yeye ndiye aliyekukosea ama KUJISAMEHE kama Wewe ndiye uliyekosea.

Mazungumzo yenu kuhusu kusameheana siyo pekee yanayoamua Wewe Kusamehe ama Kujisamehe. Hii ni kwa sababu Msamaha ni binafsi mno. Ni kwa ajili yako wewe binafsi, wewe mwenyewe. Haijalishi huyo mtu wa pili amefanya nini ama hajafanya nini. Ni wewe unashughulika na moyo wako mwenyewe.

Kwa hiyo uwepo wa aliyekukosea ama uliyemkosea mchango wake si muhimu sanaaaa kuliko msamaha wenyewe. Uhakika wa kwamba umesamehe ama umesamehewa unatoka ndani yako na siyo kwa huyo wa pili.

Hembu fikiri kama ndiyo ameshakufa sasa, utapataje huo uhakika ikiwa unategemea huyo mtu akupe uhakika.?? Hujui yupo wapi wala hutegemei kumpata karibuni, Je uendelee kubeba uchungu na maumivu moyoni mwako hadi utakapompata? Je, kwa sababu tu hapatikani uendelee kumbeba moyoni, ulale na kuamka nae, utembee na mtu umembeba kila unapoenda? Hapana. Msamaha ni wako binafsi, wewe mwenyewe..!!

Endelea kufikiria itakuwaje ikiwa uliyemkosea hataki na bado ana kinyongo? Utaendelea kuwa na uchungu na maumivu hadi atakapokuwa tayari kwa msamaha? Je akiendelea hivyo hivyo mpaka anakufa itakuwaje?

Mara nyingi Msamaha unahitaji mtu mmoja tu kuufanya uwe msamaha. Lakini Usuluhishi/Upatanisho unahitaji mtu zaidi ya mmoja, na wakati mwingine hata wa tatu ambaye atakaa kuwasuluhisha na kuwapatanisha. Ila ni kweli pia kuifikia hatua ya Usuluhishi/Upatanisho NI LAZIMA Msamaha utangulie. Haiwezekani kuanza Usuluhishi/Upatanisho kabla kwanza ya kusamehe.

Msamaha hauwi Msamaha kwa sababu tu aliyekosa amekiri kukosea, hapana. Hiyo si maana ya msamaha. Msamaha ni kuacha kuwa na uchungu na maumivu moyoni mwako. Msamaha ni kutaka kuwa na amani ndani yako. Sasa Yesu anaposema uende kupatana na adui yako haina maana kila utapoenda utakuta naye ana mwitikio mzuri kwa hatua hiyo. Unaweza kwenda kutaka kupatana na kuombana msamaha lakini yeye akasitasita ama akakataa kabisa. Swali ikishindikana tunafanyaje? Unaendelea kuhuzunika pamoja nae? Unaendelea kumsubiri hapo hadi atakapojisikia kutaka kupatana? Jibu ni hapana...

Ndiyo sababu ni wazi kabisa ukienda kusoma andiko hilo limesema nenda "ukapatane" na adui yako siyo nenda "ukasameheane" na adui yako. Kupatana hapa ni ile ya reconciliation (usuluhisho/upatanisho). Unapaswa kwenda kutengeneza. Mnatengeneza yale yaliharibika kati yenu nyie wawili. Ni hatua muhimu sana hii pia. Huwezi kusema si ya muhimu. Lakini ni ukweli pia kwamba siyo mara zote mnaweza kuifikia. Sasa mkifanikiwa kufika hapo ni jambo jema zaidi. Lakini isipofikiwa pia bado una nafasi ya kusamehe na kuweza pia kuamua kuendelea kutafuta nafasi ya kutengeneza ama kupatana wakati moyo wako tayari umeshaachilia yale maumivu na uchungu.

#SameheIshiSalama

Goodluck Ernest
+255713 660921
mashambo.ge@gmail.com
Previous
Next Post »